Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini Tanzania, Jaji
Joseph Warioba amesema iwapo Mfumo wa Serikali Tatu utaridhiwa na
wananchi ni lazima mambo yaliyo ndani ya Muungano yatagawanywa ikiwa ni
pamoja na Ikulu ya Rais. Amesema kutokana na taifa kufanya mabadiliko ya
Katiba ni lazima kuwepo mpangilio wa kugawana mambo mbalimbali
yaliyokuwa chini ya Muungano ikiwamo majengo, wafanyakazi, Ikulu, hata
vitendea kazi na kwamba utaratibu huo ni kama ule uliotumika wakati
Tanganyika na Zanzibar zilipoungana. Kauli ya hiyo ya Jaji Warioba
imekuja siku tatu tangu Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe
kueleza kuwa Tanzania Bara itaanza mchakato wa kutunga Katiba yake
Aprili mwaka 2014 na kumalizika Desemba mwaka huohuo. Jaji Warioba
aliyasema hayo katika mahojiano maalumu na waandishi wandamizi wa habari
jijini Dar es salamu, Tanzania. Hata hivyo aliongeza kuwa suala hilo
linahitajia mazungumzo ya pande zote mbili, baada ya kukamilika kwa
mchakato huu kwa sababu hii ni rasimu tu, ambayo itajadiliwa na wananchi
kabla ya kuanza kwa Bunge la Katiba na baadaye kuwepo kwa kura ya
maoni.
No comments:
Post a Comment